KAMPENI MPYA YA JIHUDUMIE YA NMB YAZINDULIWA NCHINI
Benki ya NMB imezindua Kampeni mpya ya JIHUDUMIE lenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa haraka wa huduma mbali mbali za Benki hiyo. Akizindua Kampeni hiyo jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bwana Mark Wiessing alisema mbali ya upatikanaji wa huduma ya haraka, Kampeni hiyo itawezesha huduma kupatikana muda wowote na mahali popote mteja atakapohitaji huduma hiyo.
Sasa wateja wa NMB wanaweza kupata huduma bila kwenda katika tawi
la NMB. “Tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kwamba sasa wanaweza kupata
huduma za kibenki kupitia simu za mkononi na njia nyingine mbadala kama
mashine za ATM, huduma za benki kwa njia ya intaneti, PesaFasta na
Akaunti ya Chap Chap,” alisema Wiessing.
Kupitia kampeni hiyo, NMB imeweza kuzingatia mahitaji ya msingi ya
wateja wake, ikiwemo uhakika wa huduma za kibenki na uwezo wa kuzipata
wakati wowote na mahala popote.
“Kwa kubonyeza tu kitufe cha simu, fedha itaweza kutoka kwenye
akaunti yako ya NMB kwenda mahala pengine popote kama vile kwenye malipo
ya LUKU, kulipia muda wa maongezi wa simu na hata kuweza kutoa kiasi
kinachofikia shilingi milioni moja kupitia mashine za ATM,” alisema.
Baada ya uzinduzi huo mwendelezo ulifanywa kwa matawi yote ya
benki hiyo jijini Dar es Salaam, wateja wa benki hiyo walisifia kampeni
hiyo, wakisema imelenga kuwapunguzia adha, usumbufu na kuokoa muda wa
kupata huduma za kibenki.
![]() |
Afisa Mkuu wa Huduma kwa Wateja Wakubwa wa NMB
Bw. Richard Makungwa akiwapa maelezo wateja kuhusu huduma wa Jihudumie katika
tawi la NMB Magomeni.
|
No comments:
Post a Comment