TAARIFA YA ZIARA YA RAIS KIKWETE NCHINI UINGEREZA
|
TAARIFA
KWA UMMA
Uingereza inajivunia kuwa nchi inayoongoza katika uwekezaji nchini Tanzania na itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kiuchumi na kuleta maendeleo .
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amemuambia Rais Kikwete wakati wa
mazungumzo yaliyofanyika 10 Downing Street, Leo tarehe 31 March, 14, ambapo
ndipo yalipo Makao Makuu ya Waziri Mkuu wa Uingereza.
"Tunafurahia sana uhusiano wetu na kujivunia kuwa tunaongoza katika
Uwekezaji nchini Tanzania" Bw. Cameron amesema na kumhakikishia Rais
Kikwete kuwa Uingereza iko tayari kutoa misaada zaidi.
Rais Kikwete amewasili nchini Uingereza tarehe 30 Machi, 2014 kwa ajili ya
ziara ya kikazi ya siku 3 kufuatia mualiko wa Bw. Cameroon ambaye pia amemuomba
Rais Kikwete aendelee kutoa mchango wake wa mawazo katika masuala ya kimataifa
hasa baada ya mwisho wa muda wa malengo ya millennium ya 2015.
"Tunakaribia mwisho wa muda wa malengo ya millennia Mwaka 2015, tutahitaji
kuweka vipaumbele vingine baada ya hivyo kama kuondosha umaskini, Maji safi na
salama, masuala ya ufisadi na utawala bora, natumaini utaendelea kutoa mchango
wako baada ya malengo hayo kufikia tamati" Waziri Mkuu Cameron amemuambia
Rais Kikwete ambapo Rais amekubali ombi hilo na kuahidi ushirikiano wake.
Mapema leo asubuhi Rais amekutana na mtoto wa Mfalme Prince Andrew katika
makazi ya Malkia ya Buckingham ambapo wamebadilishana mawazo kuhusu mambo
mbalimbali ya Kimataifa na Kijamii.
Kabla ya kwenda Buckingham Rais amefungua mkutano kuhusu uwekezaji na kuelezea
fursa na nafasi zilizopo za uwekezaji nchini Tanzania na kuelezea kwanini
wawekezaji watakuwa wanafanya uamuzi bora kwa kuwekeza Tanzania kuwa ni pamoja
na;
"Fursa nyingi, amani, usalama, soko la kutosha na kubwa kwa vile Tanzania
iko katika Umoja wa Afrika Mashariki, Ukanda wa Maziwa Makuu na Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika,hivyo kuwa na uhakika wa soko kubwa na
pana" amesema.
Katika ziara yake Rais pia amekutana na Mstahiki Meya wa Jiji la London Mama
Alderman Fiona Woolf na kukaribishwa rasmi Jijini London. Mstahiki Meya
anatarajia kutembelea Tanzania, Mwezi Septemba Mwaka huu.
Rais alipowasili London tarehe 30 Machi,2014, alikutana na Watanzania wanaoishi
nchini Uingereza na kuwaeleza maendeleo yaliyopo nchini Tanzania.
Rais anaendelea na ziara yake nchini Uingereza
Mwisho.
Imetolewa na;
Premi Kibanga.
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
London Uingereza
31 Machi, 14
No comments:
Post a Comment