Marmo Advert Banner

Royal Tughimbe Hotel

investment forum

investment forum

MACHEMBA STORE

MACHEMBA STORE

MBEYA SPRING WATER

MBEYA SPRING WATER

MADARAKA AUTO GARAGE

MADARAKA AUTO GARAGE

Saturday, 22 March 2014

SULTAN AWAASA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA NYINGI ZILIZOPO KWENYE UCHUMI WA GESI

Bw. Sultan A. Sultan akitoa mada wakati wa kongamano la viongozi lililojadili mada kuu isemayo ‘Rasilimali za Taifa kwa amani na Maendeleo, Bagamoyo , Pwani  tarehe 20 Machi,2014
 
 
============================================================
 
Watanzania wameaswa kutambua fursa zitokanazo na rasilimali zinazogunduliwa nchini ili waweze kunufaika kutokana na uwepo wa rasilimali hizo.

Hayo yamebainishwa na Bwana Sultan Sultani mkazi wa kilwa alipokuwa akitoa mada juu ya ‘‘Ushiriki wa wenyeji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia’’, katika Kongamano la Viongozi lililojadili mada kuhusu  “Rasilimali zetu za gesi asilia, mafuta na madini kwa amani na maendeleo ya Tanzania” lililofanyika Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Bw. Sultani alieleza kuwa, wananchi wanatakiwa kuelewa fursa mbadala zipatikanazo kutokana na uwepo wa rasilimali za gesi na mafuta nchini zikiwemo ununuzi wa hisa  kwa makampuni makubwa ili kuwawezesha kuongeza  mtaji yao  ambapo faida yake itapatikana mara tu baada ya gesi kuanza kuuzwa.

Aidha, alitaja fursa nyingine kuwa ni uwezekano wa uhitaji mkubwa wa majengo na maghala yatakayohitajika kwa ajili ya kutunza vifaa na pembejeo muhimu kwa ajili ya utafutaji na uzalishaji wa gesi katika maeneo yaliyoko baharini.

Alizitaja fursa nyingine kuwa ni pamoja na makampuni ya ulinzi, kampuni za usafirishaji, maabara, vyuo maalumu vya kuelimisha umma katika tasnia ya petroli na nyanja zake, makampuni ya kutunza mazingira, usalama na afya, na kuongeza kuwa  hizo ni baadhi tu ya fursa zitokanazo na uwepo wa rasilimali gesi na mafuta nchini. 

Pamoja na hayo, alieleza uwekezaji katika mafuta na gesi si bahati nasibu ya kutoa moja ukapata milioni moja bali ni ile ya kutoa mamilioni kama sio mabilioni na kisha ukaambulia patupu. Hivyo, alisisitiza kuwa, mifano ipo ya watu walionunua leseni za utafiti kwa kuwekeza mabilioni wakaishaia kukosa na matokeo yake wakapoteza maisha kwa maradhi ya moyo au msongo wa mawazo.

“Pamoja na kuwa sayansi ya hali ya juu kutumika katika utafiti wa mafuta na gesi, bado kwa kiasi kikubwa ugunduzi wa rasilimali hizi ni wa pata potea huku uwekezaji wake ukiwa ni wa ghali sana” aliongeza Sultan.

Alisisitiza kuwa, yapo makampuni mbalimbali yaliyofika nchini ili kuwekeza katika maeneo ya Songosongo (Lindi) na Msimbati (Mtwara) ambapo mengi yaliingia kwa kifua mbele lakini yakatokea kwa mlango wa nyuma kutokana na ugumu wa kazi hiyo na kufanya utafiti bila ya mafanikio.
Mwisho Sultan alihimiza umuhimu wa wananchi kuelezwa mapema ugumu na pata potea iliyopo katika sekta ya mafuta na gesi  ili wananchi waweze kuzitambua fursa na  kujihusisha katika kuanzisha biashara katika maeneo mbalimbali ili waweze kutoa huduma kwa wawekezaji wanaofanya utafiti na wale wanaoendelea na shughuli za uchimbaji wa gesi asilia, ikiwemo  elimu ya soko la hisa ili iweze kuwasaidia wananchi kuwekeza katika makampuni ya mafuta katika namna ambayo itawanufaisha.

No comments: